Hongera Idhaa ya Kiswahili ya DW kwa kutimiza miaka 60 ya
kuhudumia wakazi na wasikilizaji wa Afrika Mashariki na Kati.
Wakati mtangazaji wa DW Josephat Charo akihitimisha kipindi
maalumu cha MAONI katika kuadhimisha miaka 60 mnamo Februari Mosi, 2023
alisema, “Mohammed Abdulrahman
tukamilishe kipindi chetu, Februari Mosi mwaka 1963 matangazo ya Kiswahili yalizinduliwa
rasmi yakilenga eneo la Afrika Mashariki na Kati, yalizinduliwa mwaka uliokuwa
na makubwa ya kihistoria; Hotuba ya Rais wa Marekani wakati huo John F. Kennedy
katika jiji la Berlin ambalo lilikuwa limegawanyika wakati wa enzi ya vita
baridi; Kenya ni mwaka huo huo ilipata uhuru wake mikononi mwa Mwingereza na
Rais wa kwanza JomoKenyatta akaja na kauli mbiu yake, wito wake wa harambee na
hapa nchini Ujerumani akachaguliwa Ludwig Erhard kuwa kansela wa pili tangu
kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia. Maandamano ya Luther King kwenda
Washington kule Marekani na hotuba yake ‘I have a Dream’ au Nina Ndoto au Nina
Matumaini. Ni matumaini yapi unayaona,mustakabali wa Idhaa ya Kiswahili DW…Mohammed.”
Binafsi nikaguswa na mstari huu wakati akimtupia swali
mkongwe katika utangazaji mstaafu Mohammed Abdulrahman,
“Maandamano ya Luther King
kwenda Washington kule Marekani na hotuba yake ‘I have a Dream’ au Nina Ndoto
au Nina Matumaini. Ni matumaini yapi unayaona…..”
Kutoka katika vilindi vya moyo wangu bado matumaini yapo hai
ya kufanya kazi na DW haijalishi ni lini, kwani mpaka naandika ujumbe huu kwenu
DW nina umri wa miaka 38.
Tangu nikiwa mdogo, mara kadhaa nilikuwa pembeni ya Redio ya
Baba yangu katika masafa ya Short Wave (SW) kusikiliza taarifa za ulimwengu
kutoka Cologne.
Miaka ile ya 1990 ndoto ya kufanya kazi na Sauti ya Ujerumani
ilizidi kutiwa nguvu na watangazaji waliokuwepo wakati huo.
Kudhihirisha hilo nilipokuwa darasa la sita nakumbuka
nilinunua redio ndogo kwa mmachinga mmoja aliyekuwa akitembeza redio za kuuza
kwa shilingi 3,000/=.
Ulikuwa mwaka mzuri sana kwangu, mwaka 1997 katika kijiji cha
Lyamkena , Makambako mkoani Njombe.
Sikumwambia mama wala baba, nilimshirikisha muuza duka mmoja
aliyefahamika kwa jina la Method Kiwale anipe betri mbili za BELL akaniambia
anazo NATIONAL kwa ahadi ya kumlipa siku za usoni, akanipa.
Jioni ya siku hiyo mwezi wa saba sikumbuki tarehe; ilipofika
saa 12:00 jioni nilikuwa shambani juu ya kichuguu kusikiliza matangazo ya Sauti
ya Ujerumani-Cologne; yalipoisha nilizima kiredio changu na kukificha kwa
umakini mkubwa chumbani.
Nilijiambia nafsini mwangu nitakuja kufanya kazi na Sauti ya
Ujerumani. HAIJATIMIA BADO LAKINI MATUMAINI YAPO HAI.
Katika kipindi cha maoni sikumfaidi sana Othman Miraji huenda
muda mwingi nilikuwa shule lakini vizuri nimemfaidi Mohammed Abdulrahman katika mada tofauti tofauti. Kwa sasa namfaidi
Mohammed Khelef na wengine. Kwa ujumla wengi wananikosha na kujihisi
wamenizunguka na kuniaminisha kuwa inawezekana siku ndoto itakuwa kamili.
Nikiwa kidato cha sita huko Tabora Boys miaka ile ya
2003-2005 niliwahi kutuma barua kwa njia ya Posta kutokana na swali
lililoulizwa nakumbuka lilihusu klabu ya soka Manchester United, sikujua kama
barua ilifika au la … lakini nilifurahi nilipotuma DW kwa anwani waliyoitaja nami
kubandika stempu kisha kuitumbukiza katika sanduku la Posta mjini Tabora.
Utaratibu wa kununua viredio vidogo uliendelea hata
nilipokuwa Tabora kutokana na hamasa ninapoisikiliza DW.
Kwa mara ya kwanza kuonana na mtangazaji wa DW wakati huo akiwa
ni ripota ni HAWA BIHOGA nilifurahi
sana,hiyo ilikuwa mwaka 2017.
Nilikutana naye katika Mkutano wa Wanahabari wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) pale Kinondoni-Dar es Salaam wakati huo
nikifanya kazi KISS FM.
Nikamuuliza ninaweza kuzungumza na Iddi Sessanga? Akaniuliza kwanini,
nikamweleza…” Sauti yake inanishangaza sana”. Akampigia simu tukiwa tunaelekeza
studio za Kiss FM maeneo ya Morocco-Kinondoni.
Nikazungumza na Iddi Sessanga moja kwa moja nikafurahi sana
na kuyaona matumaini yangu yanazidi kukaribia huko…ila sijui lini nitafika DW…
“I have a Dream to work with DW”
Ndimi
Jabir Johnson
+255 693 710 200
0 Comments