Jabir Johnson: My Burial Day

 Siku ya Kufa Kwangu


Sina cha kujigamba, Sina cha Kuwaonyesha ila Historia Yangu... Samahani kwa Niliowakwaza, Nami nawasamehe walionikwaza; ni vema kusameheana kwasababu binadamu hatujakamilika...Naiandika mimi katika mfumo wa insha kumsaidia atakayesoma siku hiyo muhimu...

Alizaliwa siku ya Ijumaa ya tarehe 17 mwezi wa Nane mwaka 1984 kisha alipewa jina la Jabir Johnson wa ukoo wa Mking'imle; baadaye alikuwa maarufu kama Anko Tununu. Marehemu alikuwa mtoto wa tatu kati ya watano wa Zera Adams Mahalamba. Jabir alizaliwa katika Hospitali ya Kibena mkoani Njombe na kukulia maeneo tofauti mkoani humo. Babu yake alikuwa Sheikh wa msikiti wa Mtwango ambako upande wa mama yake walikuwa waumini haswa wa dini ya kiislamu wakati upande wa baba walikuwa waumini wa dini ya kikristo.

 Kiufupi katika hilo Anko Tununu alilelewa katika misingi ya imani zote mbili. Siku ya msiba huu alijua tu kuna watu watajitokeza kutaka kumiliki msiba ili kukuza dini zao, katika maelezo yake alikataa dini hizo mbili kuhusika kwa lolote isipokuwa alitaka wale wenye moyo safi wa kuamini katika Muumba wa Mbingu na Nchi na sio katika dini zao ndio wahusike akiwa na maana alioishi nao kwa furaha, amani na upendo; waliosaidiana katika raha na shida ndio hao wahusike kikamilifu. 

Kwani aliamini dini iliyosafi isiyo na unafiki ni Upendo miongoni mwa jamii hivyo anazikwa leo kwa mfumo huo jambo ambalo linawashangaza wengi kulikoni. Kwasababu Anko Tununu katika maisha yake hakupenda unafiki, alijali sana moyo wa huruma na ndio sababu mpaka anafariki dunia hakuwa na dini wala dhehebu lolote linalomjua kama muumini wake. Baada ya kuujua ukweli kuhusu dini mnamo mwaka 2013 ilikuwa mara yake ya mwisho kukanyaga katika malango ya dini hizo. 

Katika masuala ya kujisomea na kupata maarifa mbalimbali ya nafsi, roho na mwili hakuwa nyuma alipenda sana na alikuwa na uwezo mkubwa wa kuling'amua jambo bila wasiwasi. Katika suala la elimu yake alianza Shule ya msingi mnamo mwaka 1992 huko Ilembula, Njombe baadaye alihamia shule ya msingi Ikuna mwaka 1993-1994; mnamo mwaka 1995 alisoma shule ya msingi Nyamande (shule aliyoipenda sana hii, alipenda sana kuizungumzia kwamba laiti angekuwa na fedha angejenga upya historia ya kijiji hicho) Kwasababu mama yake alikuwa Mwalimu wa shule ya msingi mnamo mwaka 1996 walihamia Lyamkena sasa ni sehemu ya mji maarufu wa Makambako ambako alimalizia elimu yake ya msingi mnamo mwaka 1998. Hakika huwezi kuwa shujaa bila kufundishwa na walimu wengi. 

Of course shuleni hakuwa nyuma katika masomo lakini hakufanikiwa kufaulu darasa la saba. Wakati baba yake anafariki dunia mwezi Desemba 1998 alitamani sana kumuona akienda kidato cha kwanza lakini haikuwezekana. Baba yake alizikwa katika makaburi ya jamii pale Mtwango. 

Mnamo Januari 1999 Jabir alianza kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Mtwango wakati huo ilikuwa private school yaani ya wazazi kabla ya serikali kuichukua. Alisoma kwa bidii hadi akamaliza kidato cha nne mnamo mwaka 2002. Alikuwa miongoni mwa wanafunzi waliofanya vizuri mno katika mitihani hiyo hatua iliyopelekea kupata nafasi ya kwenda kidato cha tano yaani Advanced level. Alichaguliwa kipaji maalum Tabora Boys au wengi hupenda kuita Tabora School shule aliyosoma Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Nako huko alikuwa moto alihitimu mnamo mwaka 2005. 

Safari ya Chuo Kikuu ikiwa imeiva akachaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) akatua pale kusomea masomo ya sanaa hadi mwaka 2009 hapo hakufanikiwa kupewa shahada ikiwa imebaki miezi mitatu tu kuhitimu pamoja na wanafunzi wengine walitimuliwa kutokana na mgomo uliotokea chuoni hapo. Wakati huo Mkuu wa Chuo alikuwa Vice Chancellor Prof. Mukandala. Akaondoka kisha kujichanga tena kusoma. Akatua Mbeya ambako alijiunga na Mbeya Institute of Journalism (MIJO) kwa mwaka mmoja alisomea masomo ya Uandishi wa Habari, Utangazaji na Upigaji Picha akahitimu mwaka 2010. 

Harakati za maisha bado zikaendelea akifanya kazi na redio, magazeti na makampuni mbalimbali likiwemo EAG Group iliyokuwa chini ya Imani Kajula, (Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa Simba SC). Akiwa na EAG Group alipata fursa na experience kubwa kuliko wakati mwingine katika maisha yake. Alijifunza kujitegemea ndio msingi wa kufanikiwa badala ya kusubiri kuajiriwa hii ndio sababu mpaka wakati huu hakupenda kuajiriwa serikali na alikuwa hataki hata kidogo kuwa karibu na serikali kwa kuwa uwezo wake angechukuliwa na mfumo hivyo akawa mjasiriamali akifanya hivi na vile ili maisha yake yasonge.

Alitamani sana kuoa akiwa na umri wa miaka 25 lakini haikuwezekana kutokana na changamoto za maisha hivyo waswahili husema 'alipita na mia', mpaka anafikisha umri wa miaka 41 hakuwa na mke wala mtoto au watoto. Mpaka wakati huu hakuna ripoti yoyote iliyotolewa kuwa katika harakati zake za maisha aliacha familia sehemu yoyote hapa nchini. Inastaajabisha sana lakini huyo ndiyo Jabir Johnson maarufu Anko Tununu.....

Pumzika Anko Tununu mengine tutajaza wenyewe.....


Post a Comment

0 Comments

Total Pageviews